Sote tunafahamu kwamba CHADEMA ni chama cha siasa kilichosajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992. Kazi za chama cha siasa zimeelezwa wazi kabisa na sheria hiyo, lakini kati ya kazi nyingi zilizoainishwa na sheria hiyo, hakuna kipengele kinachoeleza kwamba chama cha siasa kinaweza kufanya kazi ya upelelezi, hasa katika mambo ya jinai.
Katika hali ya kushangaza, leo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, amefanya mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama hicho, na alichokizungumza kimetoa maswali mengi sana kwa wadau mbalimbali, hasa maswali yanayohusu mwenendo na wajibu wa chama hicho.
Ni kweli kwamba kumekuwa na taarifa za hapa na pale za upotevu na utekaji wa watu, lakini kesi zote hizi jeshi la polisi linazifahamu, na uchunguzi unaendelea kama utaratibu unavyotakiwa kulingana na taaluma na utaalamu wa kuendesha mambo hayo.
Mbowe, mbele ya waandishi wa habari, amekiri kwamba uchunguzi wa chama chake umebaini kuwa katika Kanda Maalumu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, kuna task force maalum inayohusika na utekaji huo. Mbowe anasema kwamba task force hiyo inaundwa na vyombo mbalimbali kama Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, na JWTZ.
Kauli hiyo ya Mbowe si tu kwamba ni haramu kutokana na chama kutokuwa na kazi hiyo kwa mujibu wa sheria, bali pia ni hatari kwa usalama na ustawi wa amani ya Taifa letu.
Mbowe anaposema chama chake [CHADEMA] “kimechunguza” inaleta ukakasi wa hali ya juu kwa sababu CHADEMA sio chombo cha upelelezi, wala hakina weledi wa kufanya kazi hiyo. Hivyo, kwa vyovyote vile, taarifa yoyote wanayotoa itakuwa na mapungufu mengi ya kitaalamu na hatimaye inaweza kuzua hofu kwa Watanzania.
Chama cha siasa kufanya kazi ya jeshi la polisi ni hatari na inaweza kuchochea vurugu. Ni wazi kwamba CHADEMA yenyewe inatambua hawana utaalamu wa kufanya upelelezi, hivyo dhamira ya Mbowe kufanya mkutano na vyombo vya habari ni kuichafua serikali na jeshi la polisi kwa wananchi, na kuhakikisha kwamba wananchi wanakosa kabisa imani na jeshi la polisi.
Jeshi la polisi linafanya kazi yake kwa weledi wa hali ya juu, hivyo ni wajibu wa Watanzania kuwa na subira kusubiri taarifa za kitaalamu na za kichunguzi juu ya kesi mbalimbali kutoka kwa chombo hicho chenye majukumu hayo kwa mujibu wa sheria.
Kitendo cha CHADEMA kutoa shutuma nzito dhidi ya jeshi la polisi, Usalama wa Taifa, na JWTZ kuhusika kwenye madai ya utekaji yanayoendelea nchini, kinatoa ishara na mwanga kwamba chama hicho kimepoteza muelekeo na dira hadi kufikia hatua ya kujihusisha na kazi ambazo kimsingi sio kazi za chama kwa mujibu wa sheria.