SEPTEMBA 23 YA AIBU: SABABU TANO MAANDAMANO YA CHADEMA KUANGUKIA PUA.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilitangaza kufanya maandamano waliyodai yangekuwa ya amani tarehe 11 Septemba. Hata hivyo, maandamano hayo yaliyopangwa kuwa makubwa kabisa kwenye ardhi ya Tanzania, yaliangukia pua huku mitaa ya Dar es Salaam ikiendelea kuwa salama na shughuli za kila siku zikifanyika kama kawaida. Pamoja na hekaheka za mitandaoni zilizotangulia maandamano haya, hali ilikuwa kinyume kabisa na matarajio yao.
1. Maandamano yalikuwa ya CHADEMA na sio ya wananchi.
Maandamano haya yaliandaliwa zaidi kwa maslahi ya chama kuliko maslahi ya wananchi kwa ujumla. Wananchi hawakuhusishwa vya kutosha, na kwa kiasi kikubwa yalionekana kama ni harakati za kichama zaidi ya kuwa harakati za wananchi.
2. Ajenda za maandamano hazigusi maisha ya watu moja kwa moja.
Ajenda kuu za CHADEMA zilihusisha madai ya kupinga mauaji, utekaji na ukatili. Ingawa madai haya ni muhimu, hayakugusa maisha ya watu wa kawaida kwa undani. Watanzania wengi wanajali zaidi hali ya maisha yao ya kila siku—bei nzuri za mafuta, upatikanaji wa chakula, na bidhaa nyingine za msingi. Mambo haya ndiyo huweza kuwafanya wananchi wajitokeze kwa wingi barabarani, na bila hayo maandamano hayawezi kuwa na mvuto wa kweli kwa watu wa kawaida.
3. Serikali inajua kutumia mitandao ya kijamii kwa ustadi.
Serikali iliweza kutuliza hali kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa ustadi mkubwa. Walitoa taarifa kwa uangalifu ambazo zilitumika kuwachanganya na kuwazubaisha wafuasi wa CHADEMA, ambao walikuwa na morali ya kuandamana. Mkakati huu wa kutumia mitandao ya kijamii ulilenga kupunguza morali ya wafuasi wa chama na kuwaondoa kabisa katika mawazo ya maandamano.
4. Kukamatwa kwa Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama.
Freeman Mbowe ni nguzo kuu ya CHADEMA. Kukamatwa kwake na baadhi ya viongozi wa juu wa chama kuliathiri sana uwezo wa chama kupanga na kusimamia maandamano hayo. Mbowe akiwa nje ya ulingo, chama kilianguka kimuundo na kimaandalizi, hali iliyosababisha wafuasi wengi kutotoka barabarani kama ilivyopangwa.
5. Maendeleo makubwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu.
Watanzania wameona kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu katika kuboresha hali ya maisha na kuleta maendeleo nchini. Watu wameona namna miradi ya maendeleo inavyotekelezwa kwa kasi na ufanisi. Hali hii imewafanya Watanzania wengi kuona kuwa hakuna sababu ya kuingia barabarani kwani wameridhishwa na juhudi za serikali yao.