Uzalendo ni hisia, imani, upendo na uaminifu kwa nchi au jamii ambayo mtu anatambua kama sehemu ya utambulisho wake na anajitolea kulinda na kukuza maslahi yake. Uzalendo umegawanyika katika makundi matano: uzalendo wa kijasusi na usalama, uzalendo wa kiuchumi, uzalendo wa kisiasa, uzalendo wa kijamii na kitamaduni, na uzalendo wa kimazingira.
Utaifa ni hali ya kisheria au kijamii inayomtambulisha mtu kama raia wa nchi fulani na hivyo kumpa haki za kiraia na kisiasa katika nchi hiyo. Utaifa hujumlisha wimbo wa taifa, lugha ya taifa (mfano Kiswahili ni lugha ya taifa la Tanzania), ngao na nembo ya taifa, mavazi, hati ya kusafiri, na vitambulisho vya taifa. Kwa maana ya kihafidhina, utaifa ni kitendo cha mtu kuipenda na kulisifia taifa lake huku akidharau watu au vitu vya mataifa mengine. Kwa falsafa za kinazi na kiimla, utaifa unaweza kuhusisha adhabu kali kwa watu wanaolisema vibaya taifa lao kwa kuibua uovu na udhaifu wa watawala au viongozi hadharani.
Uzalendo na utaifa ni nguzo muhimu katika ustawi na ujenzi wa taifa lenye demokrasia, ustaarabu, na misingi ya umoja na mshikamano. Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani 2024 na uchaguzi mkuu 2025, hivyo ni muhimu kuzingatia uzalendo, utaifa, umoja, na mshikamano wetu kama Watanzania.
Uchaguzi mkuu unaozingatia sheria, uhuru, usawa, na haki unapaswa kutujenga kifikra, kuongeza uvumilivu wa kisiasa, na falsafa za kukubali matokeo bila kuharibu amani, utulivu, na usalama wa nchi.
Ni muhimu kutumia lugha ya staha na kuepuka siasa za kashfa. Vyombo vya ulinzi na usalama vijiepushe na dhana au harufu yeyote ya kukipendelea na kukipigania chama cha Mapinduzi, kama ilivyotokea Zanzibar mwaka 2000 na 2015 na kupelekea mwenyekiti wa tume Zanzibar, Ndugu Jecha S. Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais.
Vijana wa ngome za vyama vya siasa kutoka vyama vyote nchini wanapaswa kujenga umoja na mshikamano, wakiachilia mbali tofauti zao za kiitikadi na mapenzi ya vyama vyao.
Tanzania ni kubwa na kongwe kuliko vyama vya siasa. Dunia nzima hakuna taifa bora kama Tanzania. Si busara kuchafua na kuvuruga amani ya nchi kwa kigezo cha kukimbilia ughaibuni—hizi ni fikra za kitumwa tunapaswa kujikemea ili kwa pamoja tujenge taifa letu kwa maslahi mapana ya vizazi vya sasa na baadaye.
Hitimisho
Jumuia ya Afrika Mashariki inaitazama Tanzania kama kisiwa cha amani, upendo, na taifa lenye ustaarabu wa kiwango kikubwa. Machafuko ya kisiasa yakitokea kwa majirani zetu, mfano Kenya mwaka 2007, Burundi kuanzia mwaka 1962 mpaka 2005, na mwaka 2025, Tanzania ndio kimbilio lao. Uganda pia ilikimbilia Tanzania kufuatia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Mheshimiwa Milton Obote mwaka 1971 na baadaye kadhia ya vita ya Kagera. Kongo nao Tanzania ndio kwao tangu mwaka 1961 baada ya kuuawa kwa waziri mkuu wa kwanza wa taifa hilo, mjamaa Mwanamajumui Patrice Lumumba. Tanzania imekuwa kinara wa kutatua migogoro kadhaa ya mataifa mbalimbali Afrika.
Mungu hakuliumba taifa la Tanzania kwa bahati mbaya, bali alitaka mataifa mengine yapate faraja kupitia Tanzania. Hivyo, amani tuliyopewa na Mungu tunapaswa kuitunza maana ikitoweka, tutatumia gharama kubwa kuirejesha.