Luhaga Mpina: Bunge Limefanya Kazi yake, Waliomtuma Wamemchinjia Baharini. - Mzalendo Daily

Luhaga Mpina: Bunge Limefanya Kazi yake, Waliomtuma Wamemchinjia Baharini.

0
98

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limempa adhabu kali Mbunge wa jimbo la Kisesa Mh. Luhaga Mpina kwa kosa la kudharau mamlaka ya Spika na shughuli za mwenendo wa Bunge.

Rekodi ya nidhamu ya Mh. Luhaga Mpina ndani ya Bunge ina dosari nyingi na inatia shaka kwani hii siyo mara yake ya kwanza kuonyesha utovu wa nidhamu kiasi cha kukanywa kutokana na matendo yake ya kutokuheshimu uongozi wa Bunge. Itakumbukwa kuwa alipokuwa akihudumu katika Baraza la Mawaziri kama waziri mifugo na uvuvi aliwahi kuingiza maafisa wa wizara yake kupima samaki kwa rula kwenye kantini za Bunge kinyume na taratibu za Bunge.

Ni wazi makosa haya ya kujirudia sio ya bahati mbaya. Kuna aina fulani ya makusudi na kiburi ndani ya Mh. Mpina mwenyewe lakini bila shaka yeyote nyuma yake pia. Ukubwa wa jeuri anayoionyesha dhidi ya mawaziri wanaotekeleza ilani ya chama chake ambayo yeye mwenyewe aliinadi, umevuka mipaka ya uungwana na ya ukosoaji.

Jitihada za Mh. Mpina kuonyesha dosari za utendaji wa baadhi ya mawaziri zinakosa ushahidi wa kimantiki. Sanasana ni dhahiri kuwa amegeuka mtu wa kutuhumu badala ya kuwa mkosoaji. Lakini kinachotia shaka ni jinsi anavyotoka kwenye kukosoa sera na mipango kwa hoja na kuanza kuwashambulia mawaziri kutokana na nafasi zao.

Ukipima kwa jicho la utulivu utagundua kuwa nyuma ya Mh. Luhaga Mpina kuna watu waliomshawishi na kumtuma kufanya haya anayoyafanya, yaliyompelekea kukumbwa na adhabu hiyo ya kukosa vikao 15 vya Bunge na kutokujihusisha na shughuli za Bunge kwa kipindi chote hicho wala kulikaribia eneo la Bunge.

Kwa kifupi, wananchi wa jimbo la Kisesa watakosa haki yao ya msingi ya uwakilishi Bungeni kutokana na Mbunge wao kushindwa kuwajibika ipasavyo, kulingana na kanuni na sheria za Bunge zinavyoagiza.

Hawa walio nyuma ya Mh. Mpina ni wazi watakua wamemchinjia baharini kutokana na muitikio wa wabunge wengine kwenye michango na kura zilizopigwa juu ya adhabu ya Mh. Mpina.

Ni wazi ni kundi lililotaka kudhoofisha ukubwa wa kazi zinazofanyika ndani ya awamu hii ya Sita, na kuonyesha kuwa uungwaji mkono ni mdogo sana kwa hatua ziliopigwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu. Lakini nia yao hiyo mbovu imefeli kabla hata haijaanza, kwani wabunge wamedhihirisha kuwa hawana mpango wa kupoteza muda kwa kujadili vioja bali kufanya mambo yenye tija na faida kwa watanzania.

Luhaga Mpina anstahili kutubu na kuomba radhi, kwanza kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambae kwa kofia yake ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, anachotokea Mh. Luhaga Mpina. Mbunge huyo wa Kisesa anapaswa kuomba radhi ya kurudisha nyuma maendeleo na jitihada za Chama chake katika utekelezaji wa ilani iliyopigiwa kura kwa kishindo. Lakini pia, Mh. Mpina anapaswa kurudi kwa wanakisesa na kuwataka radhi kwa kuwapotosha na kutokuwawakilisha ipasvyo kama jinsi alivyokula kiapo.

Mh. Luhaga Mpina anapaswa pia kuchukua muda wa kujitafakari nje ya nafasi aliyonayo, katika hali ya kujifanyia tathmini yeye mwenyewe katika anachokiamini. Muda umefika sasa wa yeye mwenyewe kumuandikia barua Mwenyekiti wa Chama chake, akimuomba kujiuzulu, kama sehemu ya uwajibikaji ili kutoa nafasi kwa watu wa jimbo lake kuchagua mtu mwenye kasi ya kuendana na Serikali ya awamu ya Sita, ambayo kimsingi, imeendelea na utekelezaji wa ilani, utekelezaji wa miradi mikubwa, kuvutia uwekezaji nchini, kuboresha huduma za afya, kuchochea utalii na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa watanzania.

Mpina ni wazi ameshindwa kuliwakilisha Bunge vyema, kwa kuonyesha utashi, weledi na maadili yanayoendana na hadhi ya Bunge. Ni wazi pia kuwa Mh. Mpina amefeli kukiwakilisha vyema Chama chake, kama chenye maono na kinachoruhusu maoni mbadala. Badala yake amekuwa akikilenga kuwa kina mienendo isiyofaa.

Kwa hatua zilizopigwa katika awamu ya sita chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania haistahili kuwa na muwakilishi wa wananchi wa aina ya Mh. Luhaga Mpina. Anavunja mioyo ya viongozi waliojitolea kulipambania Taifa letu.

Yeye mwenyewe Mh. Mpina, na wote waliokuwa nyuma yake wamefeli, wameshindwa na kuangukia pua. Ni wazi wamesambaratika na Taifa la Tanzania limeshinda vita dhidi ya waharibifu na wachochezi wasiolitakia mema Taifa letu. Mungu ibariki Tanzania.

Leave a reply